Research Papers

Permanent URI for this collectionhttps://scholar.mzumbe.ac.tz/handle/123456789/1446

Browse

Search Results

Now showing 1 - 2 of 2
  • Item
    Majuto ni mjukuu: Uchunguzi wa mhusika Ngoma katika riwaya ya ua la faraja
    (Journal of Linguistics, Literary and Communication Studies, 2024) Fuluge, Adria
    Maisha ya mtu ni hadithi inayopaswa kusimuliwa ili kutoa mafunzo kwa jamii kuhusu mapito ya mhusika. Hii inatokana na ukweli kwamba kila mtu katika jamii ana mambo mazuri na/au mabaya ya kusimulia yanayohusu mapito ya maisha yake. Yapo masimulizi yanayofurahisha kutokana na matendo ya mhusika na mengine husikitisha kiasi cha kumfanya mhusika kuyajutia maisha yake kutokana na kufanya au kutofanya jambo fulani. Kwa msingi huo, makala hii ililenga kuchunguza methali inayosema “majuto ni mjukuu” kwa kuchunguza maisha ya mhusika Ngoma katika riwaya ya Ua la Faraja (2004). Mhusika huyu ameteuliwa kama kiwakilishi cha wahusika wengi ambao katika maisha yao, walifanya na/au hawakufanya mambo fulani ambapo kutokana na kufanya na/au kutokufanya kwao, kulisababisha majuto katika maisha yao. Pia, riwaya hii imeteuliwa kama sampuli ya riwaya mbalimbali zenye wahusika wenye sifa kama za mhusika Ngoma. Data zilitokana na uchambuzi wa riwaya ya Ua la Faraja. Vilevile, Nadharia ya Uhalisia ilitumika kama mwongozo katika ukusanyaji wa data, uchambuzi na uwasilishaji wa matokeo ya utafiti wa makala hii. Matokeo yanaonesha kwamba ziko sababu kuu nne zilizosababisha Ngoma ayajutie maisha yake. Sababu hizo ni kukosa uaminifu katika ndoa, kuitelekeza familia yake, kuendekeza anasa, na kutowajali ndugu zake.
  • Thumbnail Image
    Item
    Tija za tohara kwa jamii za Kiafrika: Uchunguzi wa mhusika Omolo katika riwaya ya ua la faraja (2004)
    (Journal of Kiswahili and Other African Languages, 2025) Fuluge, Adria; Duwe, Martina
    Katika jamii nyingi za Kiafrika, tohara ni mchakato wenye thamani na tija kubwa kwa baadhi ya makabila, husuani kwa kijana wa kiume. Katika makabila hayo, asiyetahiriwa huonekana kuwa bado ni mtoto na hajakomaa kifikra na kiutu, ambapo huweza hata kutengwa katika kushirikishwa baadhi ya masuala ya kijamii. Kijana huyo kama umri wake ni mkubwa, huweza kudharauliwa na rika lake na hata waliopo chini yake. Sambamba na hilo, katika maisha halisi ya Waafrika, tohara huchukuliwa kwa thamani inayoweza kuendeleza na kuhifadhi utambulisho wa kitamaduni na kijamii. Kwao, tohara humfanya mtu atambulike kwa namna tofauti na ilivyokuwa awali. Kwa jumla, thamani ya tohara kwa Waafrika ni suala lililowashughulisha wataalamu wengi. Hata hivyo, pamoja na kuwepo kwa tafiti nyingi kuhusu tohara kwa Waafrika, bado tija za tohara kwa kufungamanisha na fasihi andishi haijamakinikiwa kwa umahususi wake. Kwa hiyo, makala hii inashughulikia jambo hilo kwa kumrejelea mhusika Omolo kutoka riwaya ya Ua la Faraja (2004). Data za matokeo haya zilipatikana maktabani kwa kutumia mbinu ya usomaji matini. Vilevile, misingi ya Nadharia ya Sosholojia ya Kifasihi imetumika katika mchakato wa kuchunguza, kuchanganua, na kuwasilisha data zilizozaa matokeo hayo. Mjadala unaonesha kwamba tohara katika maisha ya Waafrika ina tija mbalimbali kulingana na utoshelevu wa kaida zao. Makala hii inajadili tija nne; nazo ni: Kudumisha mila, kuleta heshima kwa mhusika, kujikinga na magonjwa, na kujenga ujasiri na ukakamavu.